Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imetoa msaada wa katoni 111 za taulo za kike zenye thamani ya shilingi milioni tano, kwa wanafunzi wa kike 538 walio katika kambi ya kitaaluma ya wanafunzi wa kidato cha sita mwaka 2019, inayoendelea katika Shule ya Sekondari ya wasichana Maswa Mkoani Simiyu.

Akikabidhi msaada huo, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Ziwa, Nuru Mwasulama amesema kuwa Mamlaka hiyo imetoa msaada huo kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuinua elimu mkoani Simiyu, ili kuwasaidia watoto wa kike wasome kwa uhuru na utulivu kambini hapo hususani wakati wa hedhi.

Amesema TFDA kama wadau wa mkoa wataendelea kushirikiana na Serikali mkoani Simiyu katika sekta ya elimu na masuala mengine ya Maendeleo, huku akiwasisitiza wanafunzi walio kambini kusoma kwa bidii na kutumia vizuri muda walionao  ili waweze kufikia malengo yao.

Akipokea msaada huo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ameishukuru Mamlaka hiyo kwa msaada uliotolewa kwa wanafunzi wa kike, huku akiwasisitiza wanafunzi wote walio katika kambi ya kitaaluma kusoma kwa bidii.

Aidha, Mtaka amewashukuru wadau mbalimbali ambao wameendelea kutoa michango kwa ajili ya kufanikisha kambi ya kitaaluma inayoendelea mkoani humo, huku akiahidi kuwa wadau wote waliochangia watatambuliwa na kupewa vyeti.

Katika hatua nyingine Mtaka ametoa ufafanuzi kwa wadau na wananchi kuhusu utaratibu wa kambi za kitaaluma mkoani Simiyu, kwamba kambi hizi hufanyika katika ngazi za shule na baadaye huundwa kambi moja ya mkoa kuwakutanisha wanafunzi kwa ajili ya kambi ya mkoa.

“Kambi za Kitaaluma kwenye mkoa zilianza muda mrefu lakini kama mkoa tumeweka utaratibu wa kuwa na kambi moja ya kimkoa inayounganisha shule zote za kidato cha sita; kambi za kidato cha nne nazo zinaendelea kwa hiyo tutakapofika mwezi wa saba tutaanza kuunganisha shule, kama tulivyofanya mwaka jana tuliunganisha shule 24 pale Simiyu Sekondari,” amesema Mtaka

  • Mrithi wa kiti cha Nassari apatikana CCM apatikana

Kwa upande wao wanafunzi wa kike wa Kidato cha Sita walio katika Kambi hiyo ya Kitaaluma wameishukuru Mamlaka ya Chakula na Dawa kwa msaada huo ambao wamesema utawasaidia sana kusoma kwa uhuru na kujiamini zaidi wakati wa hedhi.

TLS yapata rais mpya, Fatma Karume akabidhi kijiti
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Aprili 7, 2019

Comments

comments