Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameliagiza Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lihakikishe Tanzania inaibuka na ushindi katika fainali za michuano ya Afrika ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17 mwaka 2019.

Mashindano ya mpira wa miguu kwa Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 barani Afrika (AFCON) yanayotarajiwa kufanyika mwaka huu nchini Tanzania.

Ametoa agizo hilo Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto.

Mbunge huyo alitaka kufahamu Serikali imeyahusishaje mashindano hayo ya AFCON na mkakati wa kuendeleza utalii nchini, ambapo Waziri Mkuu amesema maandalizi yote yanaendelea kufanyika na Serikali imejiandaa vya kutosha kupokea wageni hao.

Amesema kuwa TFF inaendelea na maandalizi ya mashindano hayo ya vijana chini ya umri wa miaka 17 baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kuipa Tanzania uenyeji wa fainali hizo, amewataka Watanzania wawe wazalendo na kuipa ushirikiano timu yao ili kuhakikisha inaibuka mshindi kwenye fainali hizo.

Aidha, katika hatua nyingine, Majaliwa amesema kuwa wizara ya Maliasili na Utalii itatumia mashindano hayo kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Hata hivyo, Majaliwa amewasihi Watanzania kutumia fursa ya mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika nchini kwa kufanya shughuli mbalimbali zitakazowaongezea kipato.

Chadema walia na mshahara wa Lissu
Zaidi ya Sh. Bil. 500 zimelipwa kwa wakulima wa Korosho- Majaliwa