Shirikisho la soka nchini (TFF), limezitaka klabu zitakazoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara na ligi daraja la kwanza  kukamilisha mchakato wa usajili wa wachezaji wake kwa ajili ya msimu ujao kwa sababu muda uliopangwa hautasogezwa mbele.

Dirisha la usajili linatarajiwa kufungwa Agosti 6 mwaka huu wakati msimu mpya wa 2016/17 umepangwa kuaanza rasmi Agosti 20 kwa timu 14 za ligi kuu kushuka dimbani katika viwanja mbali mbali nchini.

Msemaji wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Alfred Lucas alisema kuwa klabu zote zinatakiwa kukamilisha usajili wake na zisitarajie kwamba muda utaongezwa kama ilivyozoeleka.

Lucas alisema kuwa uamuzi huo unatokana na muda kutoruhusu kupangua kalenda yake na kuwakumbusha viongozi wa klabu hizo kusajili kwa kutumia mfumo wa mtandao (TMS).

“Tunajua timu zinaendelea na maandalizi kwa ajili ya msimu mpya, ila tunawakumbusha msimu huu hatutasogeza mbele usajili, mwisho ni Agosti 6, tunawaomba viongozi wanaohusika na mchakato huo kuwa makini,” alisema Lucas.

Alieleza kuwa TFF iliandaa semina kwa ajili ya kutoa mafunzo ya usajili wa njia ya TMS na kila klabu iliwakilishwa na watu wawili ambao watasimamia usajili wa wachezaji.

TANZIA: Mpiga picha mkongwe Joseph Senga afariki Dunia
Simba SC Kusheherekea Miaka 80 Ya Kihistoria