Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF) limejitosa na kutoa ufafanuzi wa sakata la kiungo mshambuliaji wa Young Africans Bernard Morrison kuonyesha utovu wa nidhamu, wakati wa mchezo wa Nusu Fainali Kombe La Shirikisho dhidi ya Simba SC, uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita Uwanja wa Taifa Dar es salaam.

TFF kupitia kupitia Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB), imesema alichokifanya Morrison si kosa kisheria bali ni suala tu la utovu wa nidhamu, ambalo wanaliacha mikononi mwa uongozi wa Young Africans.

Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almas Kasongo amesema, hakuna sheria inayomzuia mchezaji kutoka nje ya uwanja na kudai alimshangaa mwamuzi wa akiba katika mchezo huo alipokuwa anamzuia kutoka nje.

“Kiujumla hajafanya kitendo cha kiungwana, alipaswa kuheshimu mashabiki pamoja na benchi lake la ufundi, lakini alishindwa pia kuwaheshimu wachezaji wenzake na kuamua kutoka nje moja kwa moja, suala hilo litaamuliwa na Yanga wenyewe,” amesema Kassongo.

Aidha, Kasongo amewataka wachezaji kuwa na nidhamu pindi wawapo uwanjani ili kujiepusha kupata lawama ambazo hazina maana kutoka kwa mashabiki wao.

Katika mchezo huo ambao Young Africans walikubali kichapo cha mabao manne kwa moja, Kocha Mkuu Luc Eymael alimtoa kiungo huyo dakika ya 79 na nafasi yake kuchukuliwa na Patrick Sibomana, lakini Morrison hakukaa katika benchi na badala yake kuamua kutoka moja kwa moja uwanjani na kuondoka.

Wakati anatoka mwamuzi wa akiba alijaribu kumzuia na kumtaka kwenda kukaa benchi na wenzake, lakini Morrison aligoma na kuondoka, jambo ambalo limezua mjadala mzito kutoka kwa wadau wa soka pamoja na vyombo vya habari, huku baadhi ya wachambuzi wakidai ni kosa kisheria.

Kagera: Ubunge CCM mchuano mkali, Majimbo Matatu 125 wachukua fomu
JPM atengua uteuzi wa Makonda na wenzake, Kunenge RC mpya Dar