Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), leo imetangaza uamuzi dhidi ya msemaji wa Klabu ya Soka ya Simba, Hajji Manara ambapo imemfungia kushiriki masuala ya Soka kwa kipindi cha miezi 12.

Akitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Wakili Jerome Msemwa alisema kuwa mbali na kufungiwa kushiriki masuala ya soka, Kamati hiyo pia imempiga Manara faini ya shilingi milioni tisa (9) ambazo anapaswa kuzilipa kabla ya kumaliza adhabu ya kifungo.

Wakili Msemwa ameeleza kuwa Kamati imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha na kumkuta na hatia Manara kwa kufanya makosa matatu dhidi ya TFF. Aliyataja makosa hayo kuwa ni kuituhumu na kuidhalilisha TFF, kueneza chuki za ukabila pamoja na kuingilia utendaji wa shirikisho hilo.

Alisema kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Soka, Manara alipaswa kupewa adhabu kali kuliko hiyo, lakini Kamati ilitumia busara na mamlaka yake kumpunguzia adhabu kwakuwa ni kosa lake la kwanza.

Hata hivyo, Wakili Msemwa alieleza kuwa Manara hakufika mbele ya kamati hiyo kujitetea ingawa taarifa za kuitwa zilimfikia yeye pamoja na Klabu yake ya Simba.

Manara amekumbwa na rungu la Kamati hiyo leo ikiwa ni takribani miezi tisa (9) imepita tangu Kamati hiyo imfungie Msemaji wa mahasimu wa Simba, wana Jangwani, Young Africans, Jerry Muro kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Muro alifungiwa kushiriki Soka kwa kipindi cha mwaka mmoja pamoja na kulipa faini ya shilingi milioni 3 baada ya kukutwa na makosa ya utovu wa nidhamu.

Breaking News: TFF Yaipokonya Simba Pointi 3 za Kagera Sugar
Video: Majaliwa awataka Mabalozi kutangaza fursa za uwekezaji Tanzania