Shirikisho la soka nchini TFF, limetoa msimamo wake kuhusu suala la klabu ya Yanga kukodishwa kwa muda wa miaka kumi kwa kampuni ya Yanga Yetu.

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mapema hii leo, katibu mkuu wa TFF Celestine Mwesigwa amesema shirikisho halijapata taarifa yoyote kuhusiana na mabadiliko yoyote katika klabu ya Yanga licha ya kusoma taarifa hizo katika vyombo vya habari.

Mwesigwa amesema TFF bado inatambua hadhi ya Yanga kubaki vilevile hadi watakapopewa taarifa rasmi na uongozi wa klabu hiyo na kuzipitia ili kuhakikisha kama kanuni na taratibu za TFF, CAF na FIFA zimefuatwa.

‘Nimewaandikia klabu ya Yanga watupe nakala za mkataba wa ukodishwaji watuelezee nini kimeuzwa, kipi kimekodishwa. Kwa sasa msimamo wa TFF ni kuwa hadhi ya Yanga iko pale pale.’

TFF wametangaza msimamo huo ikiwa ni siku kadhaa baada ya baraza la michezo la taifa BMT, kuwataka Yanga kufuata taratibu za kikatiba ili kukamilisha mchakato ambao umedhamiriwa kufanywa kupitia bodi ya wadhamini na uongozi wa kampuni ya Yanga Yetu ambayo ipo chini ya mwenyekiti Yusuf Manji.

Katibu mkuu wa BMT Mohamed Kiganja, alieleza wazi kuwa mchakato wa kukodishwa kwa klabu ya Yanga ni batili kutokana na suala hilo kutokuwa na baraka za mkutano mkuu wa wanachama na pia bodi ya wadhamini ambayo inadaiwa kusaini mkataba wa kukodishwa aliita kuwa ni batili kufuatia kuwa na wajumbe wasiotambulika kisheria.

Vifaa vya kuhakiki vyeti feki vyaibwa
Wijnaldum Amuweka Njia Panda Jurgen Klopp