Kitendo cha TFF, kurejesha michuano ya Kombe la FA inayotarajiwa kuanza mwezi ujao na kuacha nafasi moja ya uwakilishi wa michuano hiyo ya kimataifa kusalia kwa Bingwa wa Ligi Kuu Bara imeelezwa kuwa ni sawa na kuzichonganisha timu za ligi hiyo.
Kocha Mkuu wa Azam, amesema kuna ugumu mkubwa katika Ligi Kuu ya msimu huu sio kwa kikosi chake tu, bali hata Simba na Yanga na kubainisha hii inatokana na kupunguzwa kwa nafasi ya uwakilishi wa michuano ya kimataifa kupitia ligi hiyo.
Akizungumzia hali hiyo, Stewart alisema licha ya kikosi chake kushindwa kucheza katika ubora wake juzi Jumamosi dhidi ya Yanga kwa kuruhusu wapinzani wao kumiliki mpira, lakini amegundua ligi imekuwa ngumu kuanzia mwanzo kutokana na mabadiliko na kila timu kuutaka ubingwa.
Stewart raia wa Uingereza alisema kwasasa Simba, Yanga na hata Azam kila mmoja anataka kuona kikosi chake kinapata ushindi mapema kujihakikishia ubingwa mapema kwa kuwa kila mmoja anataka kukimbia mashindano ya FA ambayo ndiyo yanayotoa mwakilishi wa Kombe la Shirikisho Afrika.
“Ukiangalia msimu uliopita ligi ilikuwa inakuwa ngumu kuanzia mzunguko wa pili, duru la kwanza kila timu ilikuwa inacheza kawaida, lakini kwa sasa kila kitu kimebadilika Simba, Yanga na Azam kila moja inataka kukimbia Kombe la FA hii ni vita mpya,”alinukuliwa na Mwanaspoti.
Kocha huyo alisema Kombe la FA limebadili akili za timu hizo tatu na ndio chanzo cha Ligi Kuu kuwa ngumu na ugumu kuanza kuonekana tangu mchezo wa kwanza na mpaka sasa ikiendelea kwa sababu timu yoyote itakayozembea na kukosa ubingwa, FA itawahusu ili kupata nafasi moja iliyosalia ya uwakilishi wa nchi.

Chadema Wamshitaki Rais Kikwete Umoja Wa Mataifa Na ICC
Xavi Hernández: Natamani Kurudi FC Barcelona