Baada ya kufanikiwa kuungwa mkono na kuepuka kuangushwa katika kura ya kutokuwa na imani naye bungeni, Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May anajiandaa kuomba msaada mkubwa kutoka kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya wa kupata hakikisho juu ya mpango wake wa Brexit.

Waziri Mkuu huyo kwasasa yuko Brussels Ubelgiji anakoshiriki mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya kutafuta msaada na hakikisho kuhusu mpango wake wa kuachana na Umoja huo.

Aidha, safari hiyo ya May imekuja mara baada ya kuepuka kuangushwa katika kura ya kutokuwa na imani na uongozi wake, ambapo nchi za Umoja wa Ulaya zimefurahishwa na matokeo ya kura hiyo ingawa nchini Uingereza kwenyewe mgawanyiko unaonekana kuongezeka bungeni.

Dhamira kubwa ya waziri mkuu huyo wa Uingereza ni kutaka kuwaomba viongozi wa Umoja wa Ulaya kumsaidia katika mpango wake wa Brexit, anataka apewe hakikisho litakalomuwezesha kulishawishi bunge la nchi yake jijini London ambalo linatilia mashaka makubwa mpango wake huo.

Hata hivyo, Umoja wa Ulaya umeshikilia msimamo wake kwamba hakuna kinachoweza kubadilishwa kwa uhakika katika mpango huo wa kisheria.

 

Wizara ya Afya yatoa zawadi ya Krismasi kwa wazee
Antony Joshua ataja tarehe ya kuzichapa na Wilder