Nahodha na beki wa klabu bingwa nchini Ufaransa PSG, Thiago Emiliano da Silva amekosoa maamuzi yaliyofikiwa na viongozi wa klabu ya Man city, ya kumuondoa meneja wa klabu hiyo Manuel Pellegrini, utakapofika mwishoni mwa msimu huu.

Silva amekosoa maamuzi hayo, ikiwa ni siku mbili zimepita baada ya Man city kulazimisha matokeo ya sare ya mabao mawili kwa mawili dhidi ya PSG katika mchezo wa hatua ya robo fainali wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 31, amesema sio sahihi kwa viongozi wa Man city kufanya maamuzi ya kuachana na meneja mwenye vigezo vyote vya kukinoa kikosi chao, kutokana na makali aliyoyaona kwenye mshike mshike wa mpambano wa juzi.

Amesema huenda uongozi wa Man city ulihisi upo sahihi kufanya maamuzi kama hayo, lakini muda utawaaibisha hasa ikizingatiwa ligi ya nchini England imekua na mabadiliko ya kasi katika upinzani wa kuwania ubingwa kila kukicha.

Hata hivyo katika mazungumzo yake, Silva akugusia kabisa ujio wa Pep Guardiola, hali ambayo imedhihirisha anakubaliana na uwezo wa Manuel Pellegrini ambaye huenda akatimkia nchini Hispania.

“Ninaamini haukuwa muda sahihi kwa viongozi wa Man city kufanya maamuzi ya kumuondoa Pellegrini, kutokana na jitihada alizozionyesha msimu huu ambapo palionekana pana changamoto kubwa katika michuano yote aliyoshiriki.

“Itawauwia vigumu viongozi wa Man city, kuamini ninayoyasema sasa, lakini kwa siku za usoni watatambua ninamaanisha kitu gani, juu ya kuondoka kwa Pellegrini.’

“Ni Meneja mwenye kila sababu ya kuendelea kuwepo Etihad Stadium, nimeona uwezo na mbinu zake wakati tunacheza siku ya jumatano hapa Ufaransa, binafsi nasikitika sana kuhusu mpango wa kuondoka kwa mtu huyu.” Alisema Silva

Manuel Pellegrini ataachana na klabu ya Man city mwezi Julai mwaka huu, na tayari viongozi wa klabu hiyo ya mjini Manchester wameshakamilisha mpango wa kumuajiri Pep Guardiola ambaye kwa sasa anamalizana na FC Bayern Munich.

Salum Bausi Aipa Mtihani Mzito Kamati Ya Uchaguzi ZFA
Waarabu Wa Tunisia Kuwasili Na Ndege Binafsi