Nahodha wa timu ya taifa ya Brazil Thiago Silva, amesema hawezi kutoa ahadi ya kikosi chao kutwaa ubingwa wa dunia, lakini aameahidi kikosi chao kitacheza katika kiwango cha hali juu, kwenye michuano ya kombe la dunia itakayoanza rasmi Juni 14 nchini Urusi.

Brazil ambao bado wanakumbuka zahma ya kubamizwa mabao saba kwa moja dhidi ya mabingwa watetezi Ujerumani wakati wa fainali za 2014 zilizounguruma nchini kwao, wamekua na dhamira ya kutaka kusawazisha makosa hayo kwa kufanya vyema kwenye fainali za mwaka huu 2018.

Silva ambaye ni beki wa klabu bingwa nchini Ufaransa (Paris St-Germain) amesema, hatua ya kushiriki fainali za kombe la dunia za mwaka huu ni kubwa kwao, hivyo hawana budi kujiweka tayari kwa mapambano yatakayowakabili wakiwa nchini Urusi.

“Tuna nafasi nyingine ya kucheza fainali za kombe la dunia, hivyo tuna haja ya kuhakikisha tunacheza kwa kiwango cha hali ya juu na kuandika historia duniani,” amesema beki huyo mwenye umri wa miaka 33.

“Hatuwezi kutoa ahadi ya kutwaa ubingwa, lakini tunaahidi kupambana vilivyo katika fainali za mwaka huu na kuonyesha soka safi, japo katika faianli hizo soka safi huchezwa wakati wote.”

Kikosi cha Brazil kimeweka kambi jijini London, kikijiandaa na fainali hizo, ambazo zinasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani kote.

Marco Silva kutua Goodison Park
Urusi 2018: Nani atabeba Kombe? Tuimulike Croatia