Gwiji wa klabu ya Arsenal, Thierry Daniel Henry ameipa nafasi kubwa klabu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya soka nchini Uingereza msimu huu, endapo itamsajili mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa na klabu ya Real Madrid, Karim Benzema.

Henry ameweka wazi mtazamo wake huku baadhi ya vyombo vya habari vikiendelea kutoa taarifa za tetesi za kusajiliwa kwa mshambuliaji huyo ambaye thamani yake inakadiriwa kuwa zaidi ya paund milioni 40.

Henry amesema Banzema ni mshambuliaji wa aina tofauti ambaye ana uwezo wa mkubwa wa kufunga mabao na kama atatimiza ndoto za kucheza soka nchini Uingereza tena katika klabu ya Arsenal mambo yatakuwa mazuri zaidi msimu ujao, unaotarajiwa kuanza rasmi kesho.

Hata hivyo, gwiji huyo mwenye umri wa miaka 37 amesema ushawishi wake wa kutaka Benzema asajiliwe huko Ashburton Groove haumaanishi washambuliaji walipo The Gunners kwa sasa ni wabaya.

Amesema lengo lake ni kutaka kuona kikosi cha Arsene Wenger kinakua na ushindani wa kusaka mafanikio kwa kuona kila mmoja ana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

Hata hivyo Henry alishawahi kukaririwa na vyombo vya habari akiuponda uchezaji wa mshambuliaji wa sasa wa klabu ya Arsenal, Olivier Giroud kwa kusema haukidhi matakwa ya klabu kubwa kama Arsenal inayohitaji kushinda taji la ligi ya nchini Uingereza pamoja na barani Ulaya.

Siku kadhaa zilizofuata, Henry alikanusha kauli hiyo na kudai vyombo vya habari vilimnukuu vibaya, na badala yake alitoa ufafanuzi kwa kusema mshambuliaji huyo kutoka nchini Ufaransa anahitaji usaidizi ili kukamilisha lengo la kuisaidia Arsenal yenye uchu wa mafanikio.

Mambo Magumu Chelsea, Salah Arejeshwa Italia
Man Utd Kumjua Mpinzani Wake Leo