Nahodha na Mshambuliaji wa zamani wa Klabu ya Arsenal Thierry Henry ameitabiria makubwa Klabu ya Manchester United chini ya Meneja wake kutoka Uholanzi Erik Ten Hag.

Manchester United imeonesha kuimarika chini ya Meneja huyo aliyekabidhiwa jukumu la kuwa mkuu wa Benchi la Ufundi mwaka 2022, akitokea Ajax Amsterdam ya nchini kwao Uholanzi.

Henry ametoa kauli ya matarajio makubwa kwa klabu hiyo nguli nchini England, baada ya kuutazama mchezo wa Ligi Kuu ulioshuhudia Arsenal ikiichapa Manchester United 3-2, jana Jumapili (Januari 22) Uwanja wa Emirates jijini London.

Nguli huyo wa Soka kutoka nchini Ufaransa amesema katika mchezo huo kikosi cha Manchester United kilionesha ubora wa kupambana katika kipindi cha kwanza, na ilikua rahisi kuamini huenda kingeibuka na ushindi dhidi ya Arsenal.

Amesema kwa alichokiona kwenye kikosi cha timu hiyo, anaamini baada ya mwaka mmoja Ten Hag atakua na cha kujivunia klabuni hapo, baada ya Mashabiki wa United kusota kwa muda mrefu.

“United kwa kweli walikuwa na bora sana katika kipindi cha kwanza (dhidi ya Arsenal). Nampa mwaka mmoja zaidi kwa kocha Hag na kama atafanya usajili, United watakuwa bora sana.”

“Hakuna dharau kwa Sir Alex lakini kama Hag ataendelea hivi hivi United, watacheza soka la kuvutia zaidi kuliko walivyocheza chini ya Sir Alex Ferguson.” amesema Thierry Henry

Ushindi wa jana Jumapili (Januari 22) umeendelea kuipaisha Arsenal kileleni kwa kufikisha alama 50, United ikishuka kutoka nafasi ya tatu hadi ya nne kwa kuwa na alama 39.

Kumekucha: Rais avionya Vyama vya Upinzani
Polisi, Wananchi wafukua kaburi kupata ukweli