Mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris St Germain wamekamilisha usajili wa beki kutoka Ujerumani Thilo Kehrer akitokea kwenye klabu ya Schalke 04.

PSG wamekamilisha utaratibu huo, huku wakimsainisha Kehrer mkataba wa miaka mitano beki huyo mwenye umri wa miaka 21.

Uongozi wa klabu hiyo ya jijini Paris hadi unatoa taarifa za kukamilika kwa usajili wa Kehrer, ulikua haujaweka wazi gharama zilizotumika katika uhamisho wake, japo baadhi ya vyombo vya habari vinahisi kiasi cha Euro milioni 37 sawa na dola za kimarekani milioni 42, kimetumika katika biashara hiyo.

“Kila mmoja anaecheza soka anatamani kuwa sehemu ya klabu hii, binafsi nimefurahi kusajiliwa na PSG, ninaahidi kufanya kazi kwa kujituma ili kufanikisha malengo ya kutwaa ubingwa mwishoni mwa msimu huu,” alisema Kehrer alipohojiwa na mwandishi wa habari wa Tovuti ya PSG.

Kehrer anaondoka Schalke 04 huku akiwa na kumbukumbu ya kufunga mabao manne katika michezo 59 aliyocheza tangu mwaka 2016, akitokea kikosi cha vijana cha klabu hiyo.

Msimu uliopita alionyesha uwezo mkubwa na kuisaidia Schalke 04 kumaliza katika nafasi ta pili kwenye msimamo wa ligi ya Ujerumani (Bundesliga) nyuma ya mabingwa FC Bayern Munich.

Kwa upande wa timu ya taifa, Kehrer ni miongoni mwa wachezaji waliounda kikosi cha vijana cha Ujerumani, kilichoshiriki fainali za bara la Ulaya chini ya umri wa miaka 21, zilizofanyika nchini Poland mwaka 2017.

TRA yawafunda wafanyabiashara mkoani Geita
Video: Waziri Mkuu aagiza Mtendaji akamatwe, "Leo nalala hapa, hadi saa moja nipate majibu"