Bondia Thomas Mashali, amesisitiza kuuhitaji mkanda wa kimataifa unaomilikiwa na Francis Cheka baada ya kumchapa mpinzani wake kutoka nchini Serbia, Geard Ajetovic mwishoni mwa mwezi uliopita, katika pambano lililounguruma kwenye viwanja vya Leaders jijini Dar es salaam.

Mashali ameibuka na madai hayo kwa kuamini, Cheka hakustahili kutangazwa mshindi wa ubingwa huo, ambao upo chini ya WBF, kutokana na udhaifu mkubwa wa kupambana na mpinzani wake ambaye anaishi nchini England.

Amesema ilionekana dhahir Cheka alishindwa katika pambano hilo, ambalo lilisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa masumbwi nchini, lakini busara za uzalendo zilimbeba, na kujikuta majaji wakimtangaza mshindi.

“Cheka hakustahili kushinda hata kidogo, ushindi aliopewa ni wa dhuluma kabisa yaani nimeshangaa kuona hata viongozi wa vyama vya ngumi nao wakimtetea bila aibu” alisema Mashali

Thomas Mashali ndie bondia pekee wa Tanzania aliyebahatika kumchakaza Francis Cheka, katika pambano ambalo halikua na ubingwa, lililofanyika mkoani Morogoro, mwishoni mwa mwaka jana.

Hatua ya Mashali kutangaza kuhitaji mkanda wa Cheka, inadhihirisha yupo tayari kupanda ulingioni dhidi ya bingwa huyo wa dunia, endapo Promota atapatikana kwa lengo la kumaliza ubishi kati yao.

Rio Ferdinand: Arsenal Hawatafurukuta Kwa FC Barcelona
Arsene Wenger Awajibu Wanaotaka Aondoke Emirates Stadium