Aliyekua katibu mkuu wa Young Africans, Jonas Tiboroha amesema hana mpango wa kuwania nafasi yoyote ya uongozi ndani ya klabu hiyo baada ya kamati ya uchaguzi ya TFF kutangaza tarehe rasmi ya kufanyika kwa uchaguzi utakaowaweka viongozi wapya madarakani.

Tiboroha amesema hafikirii na wala hana mpango kujiingiza tena katika masuala ya uongozi wa klabu hiyo ambayo amekiri anaipenda na kuithamini.

Tiboroha ambaye alijiuzulu mwanzoni mwa mwaka huu katika nafasi ya ukatibu mkuu klabuni hapo, amekumbushia kauli yake aliyoitoa wakati akichukua mamuzi hayo kwa kusema kwa sasa anahitaji muda wa kufanya shughuli zake nyingine

“Nilipotangaza kujiuzulu wapo waliokuwa wakihusisha kujiuzulu kwangu na siasa, ukweli ni kwamba nilijiuzulu kutokana na majukumu niliyonayo na wala hakuna sababu nyingine” amesema Tiboroha.

Taarifa za kutoingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi zinakata kiu ya wadau wa soka nchini ambao walidhani kwamba angejitosa ili kupambana na Mwenyekiti wa Young Afrifcans aliemaliza muda wake Yusuph Manji.

Wengi walidhani wawili hao wangeingia vitan kwani mara baada ya Tiboroha kujiuzulu, Manji aliongea na waandishi wa habari katika makao makuu ya klabu ya Young Africans jijini Dar es Salaam na kusema kwamba yeye ndie aliemueleza Tiboroha ajiuzulu kutokana na madudu ambayo alikuwa akiyafanya ndani ya klabu hiyo.

Manji alisema Tiboroha alikuwa akijitengenezea umaarufu mkubwa kuliko klabu, pamoja na kuiingiza klabu katika matumizi mabaya ya fedha.

Pia alimtaka Tiboroha ajitose katika uchaguzi wa uongozi wa klabu hiyo kama angehitaji kurejea katika majukumu ya kuongoza Young Africans katika nafasi za juu za uongozi.

Chicharito Afichua Siri Ya Kujiunga Na Bayer 04 Leverkusen
Ibrahimu Akilimali: Wanachama Msichague Kiongozi Kwa Ushabiki