Khaled Mohammed, maarufu kama Top In Dar es Salaam (TID), kwa mara ya kwanza amekiri hadharani kuwa alikuwa anatumia dawa za kulevya na kuwaomba radhi watanzania kwa ujumla.

Akizungumza muda mfupi katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam muda mfupi kabla ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutaja orodha ya awamu ya tatu ya wanaotuhumiwa kwa kujihusisha na dawa za kulevya, TID amesema kuwa ameamua kuachana na dawa za kulevya na kwamba sasa anaunga mkono vita dhidi ya dawa hizo.

“Nimesimama hapa kama kijana shupavu, mpambanaji na mwenye nguvu mpya. Lakini niko hapa mbele yenu kama mnyama, narudia tena mnyama… na niko tayari kuungana na mapambano dhidi ya madawa ya kulevya,” amesema.

“Unapaswa kuwa mnyama kama kaka yangu Makonda ili uweze kuishinda,” ameongeza.

Ameongeza kuwa hakuna anayefahamu amepitia mangapi hadi kufikia hapo alipo leo na uamuzi wa kuacha dawa za kulevya akidai kuwa huenda ilihitajika nguvu ya dola kumsukuma zaidi kufikia hapo.

Aidha, mkali huyo wa ‘Zeze’ alisisitiza kuwa anataka kuwa mfano mzuri katika maisha yake, mfano mzuri kwa mtoto wake ‘Jamal’, muziki wa kizazi kipya na kwa Watanzania wote kwa ujumla.

Akizungumzia wale wanaohofia kuwa baada ya kuacha dawa hizo sasa atawataja wanaohusika na mtandao huo, alisema, “Wengine wanasema ‘yule jamaa atatutaja’, wangapi waliotajwa miaka mitatu iliyopita.”

Msanii huyo alisisitiza kuwa ameamua kuachana na dawa za kulevya na kwamba hatarudi nyuma kamwe.

TID amefikia uamuzi huo leo ikiwa ni siku chache baada ya kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kuhojiwa katika kituo cha kati cha polisi.

Siku moja baada ya kuachiwa huru, TID alionekana akiwa amemtembelea Mkuu wa Mkoa huyo na wote wawili waliweka vipande vya video vya mkutano wao kwenye Instagram.

Samson Siasia Ana Ndoto Za Kuzinoa Afrika Kusini, Rwanda
Adele akiri beyonce ni zaidi yake, ampa tuzo yake