Mlinda mlango kutoka nchini Uholanzi na klabu ya Newcastle United, Tim Krul huenda akaihama klabu hiyo na kutimkia Uhispania kufuatia mipango ya usajili inayosukwa na uongozi wa klabu ya Deportivo La Coruna.

Gazeti la El Mundo Deportivo limeandika kuwa Krul anakaribia kuondoka Newcastle Utd kutokana na kutokuwa sehemu ya mipango ya meneja wake, Rafa Benitez ambaye anatarajia kutumia siku chache zilizosalia kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili kukiboresha kikosi chake.

Krul anaaminiwa na uongozi wa Deportivo La Coruna kufuatia uwezo wake wa kukaa langoni, ambapo kwa upande wa bosi wake wa sasa Benitez haamini kama uwezo huo unaweza kumsaidia katika kampeni za kuuwania ubingwa wa England msimu huu wa 2017/18.

Hata hivyo mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 29, pia anawaniwa na klabu ya PSV Eindhoven ya nyumbani kwao Uholanzi.

Krul alikabiliwa na mtihani wa kushindwa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha The Magpies msimu wa 2016-17, hali ambayo ilimsababishia kutolewa kwa mkopo kwenye klabu ya Ajax, na mwezi Januari mwaka huu akajiunga kwa mkopo wa miezi sita katika klabu ya AZ Alkmaar.

Mwishoni mwa juma lililopita mlinda mlango huyo hakuwa sehemu ya wachezaji walioitumikia Newcastle Utd katika mchezo wa kwanza wa ligi ya nchini England msimu huu dhidi ya Tottenham.

Malalamiko Ya Klabu Katika Usajili
Eng. Ngonyani acharuka, aipa miezi mitatu TPA