Timu ya Mpira wa Miguu ya Kagera Sugar FC, inayocheza Ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara imewasili salama nyumbani Mkoani Kagera ikitokea Jijini Mwanza, Baada ya Kucheza mechi tatu za Ugenini,  na kuibuka na Ushindi mfululizo katika mechi hizo.

Timu hiyo imewasili wilayani Missenyi ilipo kambi yao usiku wa tarehe 22, na tayari imeanza mazoezi uwanja wa Kaitaba Bukoba Manispaa na kufanya mazoezi mepesi tayari kuziwinda pointi tatu muhimu dhidi ya mechi yao na wekundu wa msimbazi, klabu ya Simba ya Jijini Dar es salaam, mchezo utakaochezwa siku ya Alhamis tarehe 26,09,2019 kwa mujibu wa ratiba ya TFF.

Akiongea mara baada ya kufanya mazoezi jana, Mwalimu wa Timu hiyo,  Mecky Maxime amesema kuwa timu ipo katika hali nzuri na wapo tayari kwa mapambano huku akiongeza kuwa Simba ni timu kubwa hivyo maandalizi lazima yawe mazuri kuikabili na kutoa wito kwa  mashabiki kujitokeza kwa wingi kuipa nguvu timu yao iendeleze ushindi.

“Simba ni timu kubwa hilo halina ubishi na tunatakiwa kufanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunakabiliana nayo, namshukuru Mungu timu yangu imerejea salama na wachezaji wangu wapo salama tayari kwa kuendeleza mapambano ya kuhakikisha point 3 zinabaki, kikubwa niwaombe mashabiki na wapenzi wa timu ya Kagera sugar pamoja na wanakagara ‘kuisapoti’ timu yao na kujitokeza siku hiyo kuja kuishangilia.” Amesema Mexime.

Kagera sugar inaingia tena uwanjani Alhamisi hii kutafuta pointi tatu dhidi ya Simba huku rekodi zikionesha timu hiyo kuifunga klabu ya Simba Mara tatu mfululizo kwa mechi waluzokutana, huku timu ya Kagera sugar ikiwa imecheza michezo mitatu katika msimu huu wa Ligi kuu Tanzania bala bila kufungwa na mechi zote ikiwa imecheza Ugenini, na kuipelekea timu hiyo kuongoza ligi kwa jumla ya Pointi tisa mpaka sasa ikiwa mbele ya Namungo yenye point 7 ikiwa imecheza michezo mitatu (3) pamoja na Simba yenye point 6 ikiwa imecheza mechi mbili (2).

 

Prof Jay atuma salamu nzito kwa wasanii wa HipHop
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Septemba 24, 2019