Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Njombe mjini kimewavua uanachama na kuwafutia haki zao ndani ya chama hicho viongozi na wanachama wawili huku wanne wakipewa onyo.

Hayo yamesemwa na katibu wa chama hicho jimboni humo ambaye pia ni diwani wa Kata ya Ramadhani, George Menson Sanga ambapo amesema kuwa chama kimefikia uamuzi huo kutokana na ukiukwaji wa katiba na miongozo ya chama.

Amesema kuwa machi 8, 2018 kamati ya jimbo la Njombe mjini ilikutana kwaajili ya kujadili shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupokea na kujadili taarifa za kiutendaji za wenyeviti wa serikali za mitaa na madiwani ndani ya halmashauri ya mji wa Njombe na kufikia uamuzi huo.

“Katika hatua moja chama kimetoa onyo kwa wenyeviti wanne (4) ambao hatutawataja kutokana na kukiri kwao na kuahidi kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi,”amesema Sanga

Katika hatua nyingine amesema chama kimemsimamisha uanachama mwanachama Josephine Mabena wa tawi la Itulike shuleni kata ya Ramadhani amabye pia alikuwa ni mjumbe wa serikali ya mtaa huo.

Aidha, ameongeza kuwa uamuzi wa kumvua uanachama, Erick J Msigwa aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Melinze kata ya mji mwema kutokana na kuhusika kwake katika tuhuma mbali mbali zinazomkabili.

Hata hivyo, Sanga amesema chama kinatambua kuwa wanachama hao walikuwa na nafasi katika uongozi wa uwakilishi wa wananchi lakini kwa kukosa kwao sifa ya kuwa wanachama tayari chama kimevikumbusha vyombo vinavyohusika kutimiza wajibu wake kwa hatua za ziada ikiwa ni pamoja na kutangaza nafasi wazi ya uenyekiti katika mtaa wa Melinze.

 

Lowassa awatumia salamu Chadema, ‘msiniwekee maneno’
Video: JK aongoza maelfu kuaga mwili wa Kibonde jijini Dar