Mwanamuziki wa kike wa Nigeria, Tiwa Savage jana usiku aliandika historia ya kuwa mwanamuziki wa kwanza wa kike wa nchi hiyo kushinda tuzo za Muziki za Ulaya za MTV (MTV EMAs) katika kipengele cha Afrika, ‘Best African Act’.

Tiwa alipenya kwenye msitu wa ushindani mzito katika kipengele hicho kilichokuwa kimewataja Davido (Nigeria), Destruction Boyz na Shekinah (Afrika Kusini) na Fally Ipupa (DRC).

Akisherehekea ushindi wake, Tiwa ameandika ujumbe mzito kwenye Instagram akiwahamasisha na kuwatia moyo wanawake wote kuhakikisha wanaongeza mapambano kutimiza ndoto zao.

“Nimepitia mengi lakini nilisimama imara na kushinda kimbunga kwa sababu najua kuna baadhi ya wasichana sehemu fulani wanaota kama mimi nilivyowahi kuota,” inasomeka sehemu ya post yake ambayo pia aliwashukuru mashabiki.

Tiwa ambaye hivi sasa ni mwanafamilia wa kampuni ya Sony/ATV Music Publishing, amekuwa kwenye kilele cha muziki nchini Nigeria tangu alipoanza safari hiyo mwaka 2012 akiwa chini ya Mavin Records inayomilikiwa na Don Jazzy.

‘Aliyetisha zaidi’ kwenye tuzo hizo jana usiku akizoa tuzo muhimu ni mwimbaji Camila Cabello mwenye umri wa miaka 21. Camila alishinda tuzo katika vipengele vya ‘Wimbo Bora’, ‘Msanii Bora’, ‘Video Bora’ na ‘Msanii Bora wa Marekani’ (Best U.S Act).

Wanaume waongoza kwa kujiua
Kocha Claude LeRoy amuita tena Emmanuel Adebayor