Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) imewashauri wananchi na Mamlaka za  Miji kuhakikisha kuwa mifumo na njia za kupitisha maji katika maeneo yao inafanya kazi kwa kiwango cha kutosha ili kuepuka madhara yanayoweza kutokana na mvua za msimu zinazotarajiwa kuanza mwezi Machi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) Dkt. Agnes Kijazi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam kuhusu mwelekeo wa msimu wa mvua Tanzania katika kipindi cha mvua za masika kuanzia Machi hadi Mei.

Amesema kuwa yapo maeneo ambayo yatapata mvua za wastani na juu ya wastani na wengine chini ya wastani hivyo ni vema wananchi wakachukua tahadhari ili kuepuka madhara mbalimbali ambayo yanaweza kuwapata kutokana na mvua hizo.

Dkt. Kijazi ameongeza kuwa mvua hizo zinaweza kusababisha maji kutwama katika baadhi ya maeneo ya hivyo kusababisha mafuriko ambayo yatapelekea kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko na uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo mifumo ya maji na barabara.

Aidha ,Mkurugenzi Mkuu amesema kuwa hali ya unyevunyevu katika udongo inatarajiwa kuimarika kiasi cha uzalishaji wa malisho ya mifugo  na ukuaji wa mazao katika baadhi ya maeneo kuongezeka .

Hata hivyo , Mkurugenzi Mkuu huyo amewashauri wafugaji kuwa na mifugo ambayo inalingana na uwezo wa malisho yaliyopo kulingana na ushauri wa Maafisa Mifugo.

Dkt. Kijazi ameyataja maeneo ambayo yanatarajiwa kuwa na mvua ya wastani na juu ya wastani kuwa ni Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya na Iringa.

Maeneo ambayo yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani ni njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, na kusini mwa Morogoro.

Amesema kuwa ukanda wa Ziwa Victoria na maeneo ya Pwani ya Kaskazini mvua zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuungana na msimu wa Machi na kusambaa katika maeneo mengine.

Dkt. Kijazi amesema kuwa maeneo ya  Arusha, Manyara na Kilimanjaro , Tanga, Dar es Salaam, Kaskazini mwa Morogoro na Visiwa vya Unguja na Pemba yanatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani na vipindi virefu vya ukavu.

Yusuph Mlela aikosoa tasnia ya filamu
Mwakifamba akanusha kutuma ujumbe katika mitandao ya kijamii