Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua, katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2018 hadi Aprili, 2019.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi amesema kuwa Mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Njombe, Iringa, Ruvuma, kusini mwa mkoa wa Morogoro, Lindi na Mtwara.

Amesema kuwa maeneo ya mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, huku vipindi vingi vya mvua vikitarajiwa nusu ya kwanza ya msimu wa Novemba, Desemba, Januari, Februari, Machi na Aprili, 2018/19 na kupungua nusu ya pili ya msimu huo.

“Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2018 katika mikoa ya Kigoma na Katavi na wiki ya tatu na ya nne katika maeneo mengine yaliyosalia. Mvua zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2019 katika maeneo mengi yanayopata msimu mmoja wa mvua,” amesema Dkt. Kijazi

Aidha, kutokana na mvua za vuli katika maeneo hayo ametoa ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Wanyamapori, Maliasili na Utalii, Uchukuzi na Mawasiliano, Nishati na Maji, Mamlaka za Miji, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa.

Hata hivyo, ameongeza kuwa mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Wanyamapori Katika kipindi cha mvua za ‘Msimu’ (Novemba hadi Aprili) 2018/19, hali ya unyevunyevu wa udongo kwa ustawi wa mazao na upatikanaji wa chakula cha samaki vinatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi.

 

NEC yatangaza uchaguzi mdogo Babati na Ukerewe
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Oktoba 19, 2018