KAMATI ya Olimpiki Tanzania (TOC) imesema kuwa bado kuna muda wa kufuzu kwa wanariadha kwa ajili ya kushiriki Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo, Japan 2020.

Makamu wa Rais wa TOC, Henry Tandau ameyasema hayo mjini Kibaha mkoani Pwani  wakati akifunga kozi ya makocha wa mchezo wa Judo.

Tandau amelazimika kutoa ufafanuzi wa kufuzu kwa michezo ya Olimpiki, kufuatia kusambaa kwa taarifa ambazo ziliwahusu baadhi ya wanariadha wa Tanzania waliokwenda kushiriki michuano ya mbio za Nagai (Nagai Marathon) na kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Tokyo.

Tandau amesema kuwa bado vigezo vya kufuzu kwa michezo hiyo havijatolewa, na kwa utaratibu wanariadha watapata vigezo hivyo kupitia mashindano husika yatakayotangazwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha dunaini (IAAF) kupitia Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

Kwa mujibu wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), wanariadha wa marathon pamoja na mbio za kilometa 10 zitaanza kufuzu Januari Mosi, 2019 hadi Juni 2020 na mbio zingine pamoja na kmichezo mingine ya uwanjani kuanzia Julai Mosi 2019 hadi Juni 2020.

Tandau amesema kuwa  sio kweli kuwa kuna mwanariadha wa Tanzania ameshafuzu kwa Michezo ya Olimpiki 2020 kwani kwanza bado muda haujafika wa kufuzu na pili mbio za Nagai Marathon, hazimo katika orodha ya kufuzu kwa michezo hiyo.

Hivi karibuni taarifa zilieleza kuwa mwanariadha Angelina John aliyeshiriki Nagai Marathon zilizofanyika Japan alifuzu baada ya kumaliza wa kwanza katika mbio za marathon Oktoba 21.

Taarifa iliyotolewa na mwanariadha wazamani na mjumbe wa Kamati ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Juma Ikangaa ilisisitiza kuwa mwanariadha huyo amefuzu kwa ajili ya Olimpiki.

Tandau alisema kuwa mashindano hayo hayatambuliki ila wanariadha hao wangeweza kuyatumia kama mazoezi kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kimataifa, ambayo yataorodheshwa kwa ajili ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki 2020.

Mbali na Ikangaa, Mkurugenzi wa Maadhimisho ya Taifa, Mohamed Kiganja ambaye alikuwa  mkuu wa msafara huo aliwashukuru wanariadha hao kwa kufanya vizuri na kusema kuwa mbio hizo hazikuwa na washiriki wengi kama zilivyo mbio zingine.

Majaliwa adai Tanzania hakuna ubanaji uhuru wa vyombo vya habari
Trump avalia njuga mauaji ya mwandishi Saudi Arabia