Mbunge wa Jimbo la  Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) jana alijikuta kikaangoni dhidi ya mawakili wa upande wa wadai katika kesi ya kupinga matokeo ya ubunge kupitia uchaguzi wa Oktoba 2015 yaliyompa ushindi dhidi ya Stephen Wassira (CCM).

Mawakili hao walimbana Bulaya kuhusu tofauti ya idadi ya wapiga kura iliyoonekana katika fomu ya matokeo namba 24B iliyoandikwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo na ile iliyoonekana katika kiapo chake alichowasilisha mahakamani.

Bulaya alidai kuwa Fomu namba 24B aliyopewa na msimamizi wa uchaguzi ilikuwa na idadi ya wapiga kura 69,369 lakini aliyokuwa nayo Msimamizi baada ya kujumlisha kura zote ilikuwa na jumla ya wapiga kura 69,460.

Alipotakiwa kueleza ni ipi idadi sahihi kati ya inayoonekana kwenye kiapo chake na ile iliyo kwenye fomu namba 24B ya msimamizi wa uchaguzi, alidai kuwa hakuweza kujua ipi sahihi kwani wakati msimamizi anaandika idadi hiyo baada ya kujumlisha matokeo yote yeye alikuwa mbali hivyo hakuweza kuona. Aliongeza kuwa ingawa hakuweza kuona, aliamini alichoandika msimamizi huyo wa uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Lucy Msofe kilikuwa sahihi.

Mawakili hao walimbana tena Bulaya kuhusu namna alivyoweza kufahamu idadi kamili ya wapiga kura wa wilaya nzima ambao ni 164,794 wakati hakuweza kujua idadi sahihi ya wapiga kura katika baadhi ya majimbo, alisema kuwa aliweza kufahamu idadi hiyo kwa kusoma takwimu kabla ya kuanza uchaguzi kwani taarifa hizo sio za siri.

Aidha, Bulaya alisisitiza kuwa tofauti ya idadi ya wapiga kura inayoonekana kwenye nyaraka hizo 69,460 na 69,369 ni ndogo sana hivyo haiwezi kuathiri uchaguzi wa jimbo hilo.

Kesi hiyo ya kupinga matokeo iliyofunguliwa na wapiga kura wanne katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza inaendelea kusikilizwa mjini Musoma chini ya Jaji Noel Chocha.

Asilimia 90 ya maoni muswada wa habari yafanyiwa kazi
Mauricio Pochettino: Moussa Sissoko Alimpiga Arter Kwa Makusudi

Comments

comments