Shirikisho la soka barani Afrika CAF, limeshikilia msimamo wake wa kuitaka timu ya taifa ya Togo, kucheza mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika za mwaka 2017, nchini Tunisia dhidi ya wenyeji wao, licha ya kuibuka madai ya wasiwasi wa kiusalama.

CAF wameendelea kutangaza msimamo huo kwa Togo, kufuatia viongozi wa soka nchini humo, kuliandikia barua shirikisho la soka barani Afrika, kwa lengo la kueleza wasiwasi wao kuhusu vurugu na mashambulizi yanayoendelea nchini Tunisia.

Katibu mkuu wa shirikisho la soka nchini Togo, Pierre Lamadokou, amekaririwa akisema kwa kuwa CAF wamewalazimisha kucheza mchezo wao nchini Tunisia, hawana budi kufanya hivyo, lakini akatoa angalizo wa kuhakikishiwa usalama watakapokua ugenini.

Kauli hiyo ya Lamadokou, inadhihirisha shirikisho la soka nchini Togo limekubali kwa shingo upande amri ya kuelekea nchini Tunisia, kucheza mchezo huo, utakaounguruma kati kati ya juma lijalo katika mji wa Monastir.

Togo inaongoza msimamo wa kundi la kwanza kwa kufikisha point 6, zilizotokana na ushindi katika michezo yao miwili iliyopita dhidi ya Liberia waliokubali kufungwa mabao mawili kwa moja pamoja na Djibouti waliofungwa mabao mawili.

Tunisia katika kundi hilo anashika nafasi ya tatu kwa kuwa na point 3, zilizotokana na ushindi wa mchezo wao wa kwanza dhidi ya Djibouti ambao walikubali kufungwa mabao manane kwa moja, na katika mchezo uliofuata Eagles of Carthage waliambulia kisago cha kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya Liberia.

Arsene Wenger Awajibu Wanaotaka Aondoke Emirates Stadium
Man City Yaandika Historia Etihad Stadium