Taarifa tulizozipata zinaeleza kuwa Kambi ya Ukawa imepanga kuzindua rasmi kampeni yake walioyoipa jina la ‘Toroka Uje’, ikiwa na nia ya kuhamasisha watu wengi kukitoroka Chama Cha Mapinduzi na kumuunga mkono mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa chanzo chetu, baadhi ya majina ya vigogo wa CCM wanaodhaniwa kuwa huenda wakajiunga na kambi ya upinzani kupitia kampeni hiyo ni pamoja na mwana siasa mkongwe, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru.

Wengine wanaotajwa kuwa huenda wakajiunga na Ukawa ni pamoja na waziri asiyekuwa na wizara maalum, Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Sophia Simba na Balozi Juma Mwapachu.

Hata hivyo, Sophia Simba ambaye aliwahi kupinga wazi uamuzi wa Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM kulikata jina la Edward Lowassa, aliwahi pia kukanusha kuwa na mpango wa kumfuata mwanasiasa huyo katika kambi ya upinzani.

Jina la Profesa Mark Mwandosya na Mzee Kingunge ni kati ya majina ya watu waliopinga waziwazi uamuzi wa CCM kulikata jina la Lowassa kwenye kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea urais, ambapo Dk. John Magufuli alichaguliwa kati ya wagombea 42.

Profesa Mark Mwandosya aliwahi kusikika akieleza kuwa wajumbe wa kamati ya Usalama na Maadili pamoja na mwenyekiti wa Kamati hiyo ya CCM walikuwa na majina yao mfukoni.

Baada ya kujitokeza hadharani kupinga uamuzi wa CCM, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ulimvua madaraka aliyokuwa nayo katika umoja huo kwa madai ya kutokuwa na imani naye baada ya kukiuka taratibu za chama.

Tuendelee kusubiri matokeo ya kampeni ya ‘Toroka Uje’ ya Ukawa, huku tukisubiri pia matokeo ya kampeni ya ‘Nimeshtuka’ ya CCM, zote zikiwa na lengo moja la kusomba wafuasi wa vyama.  Je, nani atavuka kwenda ng’ambo ya mto? Majibu yatapatikana hivi karibuni kwani zimebaki siku 25 tu.

Chadema Waililia Tena NEC, Jaji Lubuva Asema Wanawapa Shida
Van Gaal Akaliwa Kooni Na Mkewe