Mabingwa wa Soka Tanzania Bara  Simba SC wametangaza vita dhidi ya mabingwa wa soka barani Afrika Al Ahly kuelekea mchezo wa mzunguuko wa pili wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Simba SC wametangaza vita kwa kuipachika jina ‘TOTAL WAR, POINT OF NO RETURN’ kupitia kwa mkuu wa idara yao ya habari na mawasilino Haji Sunday Ramadhana Manara, alipozungumza na waandishi wa habari leo mchana jijini Dar es salaam.

Manara amesema wanafahamu wapinzani wao wanapewa nafasi kubwa ya kuibuka ana ushindi kwenye mchezo huo ambao utachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam, mishale ya saa kumi jioni, lakini Simba SC haipo kinyonge kwa kukubaliana na hilo kirahisi.

“Mabingwa wa Afrika Al Ahly ambao wametoka kushiriki ubingwa wa dunia na kushika nafasi ya tatu watakuja kuwakabili mabingwa mara nyingi zaidi wa Afrika Mashariki ambao ni Simba.”

“Rekodi hizo zitaufanya mchezo kuwa wa kipekee ndani ya uwanja na kila mmoja ninatambua kwamba anajua namna ambavyo tunahitaji ushindi.”

“Mara ya mwisho tulikutana hapa Dar tukawafunga  1-0 kwenye mechi tuliyosema “YES WE CAN” na tukaweza na mara zote tukicheza Tanzania tunawafunga.”

“Al Ahly sio timu nyepesi. Tunaposema tunaweza kuwafunga tunajua ukubwa wao, lakini Simba hupenda mechi kubwa kama hizi.”

“Mechi ya mwisho tuliita WAR IN DAR, mechi ya jasho na damu ndani ya dakika 90 na sasa tunasema TOTAL WAR : POINT OF NO RETURN hii sasa ni vita kamili ya ndani ya uwanja.” Amesema Manara.

Al Ahly inaongoza msimamo wa ‘Kundi A’ kwa kuwa na alama tatu sawa na Simba SC, lakini tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa inazitenganisha timu hizo.

Al Ahly alishinda mchezo wake uliopita dhidi ya El Mereikh ya Sudan kwa mabao matatu kwa sifuri, huku Simba SC ikiichapa AS Vita Club ya DR Congo bao moja kwa sifuri.

PICHA: Clube Deportivo 1° de Agosto waanza safari ya Bongo
Ngorongoro Heroes mtegoni tena AFCON U20