Rais wa Kamisheni ya Kusimamia na Kuratibu Ngumi za Kulipwa nchini Tanzania ‘TPBRC’ Palasa Chaurembo, amesema wapo nyuma ya Bondia Mfaume Mfaume kuelekea pambano lake la Kimataifa dhidi ya Bondia kutoka nchini Misri Abdumonem Said.

Palasa aliyeingia madarakani siku kadhaa zilizopita amesema kiu kubwa ya Uongozi wa TPBRC ni kuona Mfaume Mfaume anafanya vizuri katika mchezo huo, unaosubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa Masumbwi nchini kote.

Amesema TPBRC ipo pamoja na Gym ya Nakoz anayofanyiwa mazoei Bondia huyo ambaye kwa kipindi kirefu alikua kimya, ili kufanikisha lengo la kutamba ulingoni siku hiyo.

“Naipongeza Nakoz Gym, pia nawapongeza wadau wote wa mchezo wa ngumi nchini, TPBRC tupo nyuma ya Mfaume Mfaume kwa sababu tunaamini akishinda, Tanzania yote imeshinda.”

“Mfaume Mfaume alikaa muda mrefu sana hajapanda ulingoni, naamini kwa sasa anajiandaa vilivyo ili afanikishe ushindi dhidi ya mpinzani wake kutoka Misri, TPBRC tunatimiza wajibu wetu wa kuwa naye bega kwa bega ili kumpa morari ya kufanikisha dhamira ya ushindi.”

“Mfaume aendelee kufanya mazoezi yake vizuri, awasikilize vizuri makocha wake, ili sisi wote pamoja na TPBRC tuweze kufurahia ushindi wake, kwa sababu Tanzania inasubiri huo ushindi kwa hamu kubwa.” amesema Chaurembo Palasa.

Bideni aanza ziara Korea Kusini, Japan
MZFA: CCM Kirumba imerejea kwenye ubora wake