Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati nchini Zambia, Mhandisi Himba Cheelo amefanya ziara ya kikazi kutembelea mitambo ya kupokelea Gesi Asilia Kinyerezi, inayomilikiwa na TPDC.

Akiwa eneo hilo, Mhandisi Cheelo amesema lengo la ziara yake ni kujifunza namna Tanzania ilivyopiga hatua za uzalishaji na usambazaji wa Gesi Asilia kwa matumizi mbalimbali, kama vile uzalishaji wa umeme viwandani, kwenye Magari na manyumbani.

Cheelo asema, “Zambia imefanya mabadiliko makubwa katika suala zima la uagizaji na uingizaji wa mafuta ya Petroli ambapo kufikia Septemba 30,2022 Serikali ya Zambia ilijiondoa rasmi katika jukumu la kuagiza mafuta ya petroli, na kuachia jukumu hilo Kwa sekta binafsi.”

Aidha, Cheelo ambaye alikuwa na Mwenyeji wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Heri Mahimbali ameongeza kuwa, “Ziara yetu inalenga kujifunza namna ambavyo Tanzania imepiga hatua katika suala zima la Gesi Asilia pamoja na uagizaji wa mafuta ya Petroli.”

Kwa upande wake Mahimbali alisema “tunafurahi kupokea ugeni huu na tupo tayari kuwapatia ushirikiano kwaajili ya wao kujifunza namna ambavyo Serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia imepiga hatua katika eneo la Nishati hasa Gesi Asilia, umeme pamoja na mafuta ya Petroli.”

Mhandisi Cheelo pia atatembelea kituo cha kujaza gesi asilia kwenye Magari kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam, Karakana ya DIT ya kubadili mifumo ya magari kutumia Gesi Asilia, Taasisi ya uagizaji wa Mafuta (PBPA), Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Nishati na Maji-EWURA na kampuni Tanzu ya kuzalisha nguzo za umeme za Zege inayomilikiwa na TANESCO.

Man City yashikwa pabaya, kutimuliwa Ligi Kuu
Baleke, Sakho wako vizuri, Okrah hali tete