Bodi ya Ligi Tanzania Bara ‘TPLB’ imetoa ufafanuzi wa tuzo ya Mfungaji Bora kwa msimu wa 2021/22, ambao utafikia tamati leo Jumatano (Juni 29) katika viwanja vinane tofauti.

Hadi sasa Mshambuliaji wa Mabingwa Young Africans Fiston Kalala Mayele na George Mpole wanaendelea kupambana kuwania tuzo hiyo, huku kila mmoja akifunga mabao 16.

Afisa Habari wa TPLB Karim Boimanda, amesema endapo wawili hao watamaliza msimu wakiwa na mabao sawa ya kufunga, wataangalia kanuni ambazo zinatoa ufafanuzi nani anapaswa kuwa mfungaji bora.

Boimanda amesema: Ikitokea Fiston Mayele na George Mpole watamaliza msimu na magoli kama yalivyo sasa (16), kikanuni Mayele ndiye atakuwa mfungaji bora kwa kuwa hana goli la penati wakati Mpole ana penati mbili.”

Young Africans itamaliza msimu wa Ligi Kuu 2021/22 kwa kucheza didi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku Mshambuliaji Fiston Mayele akitarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo iliyotwaa Ubingwa wa Tanzana Bara.

Geita Gold FC nayo itamaliza msimu kwa kucheza dhidi ya Coastal Union katika Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga, huku George Mpole akitarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Kocha Fred Felix Minziro.

Mataifa yahimizwa kulinda haki za wananchi
Wakili atinga Mahakamani na vazi la 'sangoma' jaji aahirisha kesi