Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ‘TPLB’ imempongeza na kumshukuru kipekee Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake kubwa katika kupigania maendeleo ya Soka nchini ndani ya miaka miwili ya uongozi wake.

Katika kipindi hicho, Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kwenye masuala yote yanayochochea ukuaji wa kiwango cha Soka ikiwemo kuweka mazingira rafiki kwa mchezo huo pendwa kuchezwa na hamasa kwa wachezaji.

Hivi karibuni Watanzania wameshuhudia namna kiongozi huyo wan chi alivyozihamasisha klabu za Simba SV na Young Africans hadi kufanikiwa kutinga hatua ya Robo Fainali ya michuano ya Afrika kwa ngazi ya klabu.

Motisha ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kila bao lililofungwa na klabu hizo, imechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio haya ndio sababu kwa nyakati tofauti viongozi na wachezaji wa klabu hizo wamemshukuru Rais Samia na kukiri jambo hilo limekuwa likiwasukuma kufanya vizuri.

Bodi ya Ligi imekiri na kuthamini ushirikiano mkubwa inaoupata kutoka serikalini kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo ambayo imekuwa pamoja na Bodi hiyo na klabu za Soka katika nyakati zote.

“Bodi inazipongeza pia klabu za Simba na Young Africans kwa kufuzu hatua ya Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho barani Afrika kwa mfuatano.”

“Hatua hii imeendelea kuliletea heshima kubwa taifa letu na mpira wetu kwa ujumla. Mchango wa wadau wote wa mpira wa miguu umekuwa mkubwa na wa kupongezwa kwani umesaidia klabu zetu kupiga hatua hii kubwa.”

“Bodi inawashukuru Mashabiki wote, Wanahabari, Wadhamini na wadau wengine waliofanya jitihada mbalimbali na inawaomba kuendeleza mshikamano katika hatua zinazofuata.” Imeeleza taarifa ya Bodi ya Ligi

Dkt. Mpango akemea mamlaka za maji kuzoea matatizo ya Wananchi
Msaada wa maafa: Rais Chakwera aishukuru Tanzania