Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa agizo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutowashughulikia wafanyabiashara waliotoa maoni yao katika mkutano wao na Rais Magufuli.

Ametoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es salaam katika mkutano wa wafanyabiashara hao na Rais John Pombe Magufuli wenye lengo kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba wafanyabiashara hao.

”Hapa nilipokuwa nasikiliza mfanyabiashara kutoka mkoani anaongelea kero za TRA, nimepata ujumbe unaosema kwamba ”Huyo anayezungumza kuhusu madudu ya TRA nakuhakikishia waziri mkuu anashughulikiwa, TRA ni miungu watu, hawakamatiki,”amesema Majaliwa

Amewataka TRA kujirekebisha kwani wamekuwa wakilalamikiwa na wafanyabiashara kwa kuwabambikia kodi mbalimbali zisizokuwa na tija yeyote, pia kuomba rushwa kitu ambacho ni kinyume cha sheria na taratibu za kazi.

”Nawaagiza TRA muache mara moja tabia hii, na mtu yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali, naagiza asishughulikiwe mfanyabiashara yeyote hapa aliyetoa kero zake kuhusu nyinyi,”amesema Majaliwa

Hata hivyo, Majaliwa amewataka wafanyabiashara hao kuendelea kuiamini serikali na itaendelea kushirikiana nao kwa karibu zaidi hivyo wasiwe na hofu yoyote na kuahidi kushughulikia kero zote.

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Juni 8, 2019
Rais Museveni amuondoa Chameleon kwenye Twitter yake baada ya kutangaza kugombea