Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeagiza maduka yote yaliyofungwa katika mikoa ya kusini Lindi na Mtwara, yafunguliwe na kuendelea kuhudumia jamii na Serikali iweze kupata kodi yake.

Hayo yamezungumzwa na Elijah Mwandumbya ambaye ni kamishna wa kodi na mapato ya ndani, pindi alipofanya kikao na wafanyabiashara mkoani Lindi.

Mwandumbya ametoa agizo hilo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wadau hao kwamba baadhi ya wafanyabiashara wakiwamo wa vifaa vya ujenzi, soda na vyakula katika mikoa hiyo, wamelazimika kuzifunga kwa madai kukadiliwa kodi kubwa tafauti na kile wanachokipata.

“Sisi TRA ni wakala tu wa kukusanya maduhuri ya Serikali, leo mnapofunga mnategemea inapata wapi fedha za kutekeleza masuala ya maendeleo kwa jamii, ”amesema Mwandumbya.

Amesema Serikali inapokusanya kodi inaiwezesha kutekeleza majukumu yake, ukiwamo ujenzi wa vituo vya kutolea huduma kwa jamii, ununuzi wa dawa na vifaa tiba, miundombinu ya mawasiliano ya barabara, umeme na nyinginezo.

Aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanaweka vizuri mahesabu yao, ili kuepuka usumbufu wa kukadilia kiwango kikubwa cha kodi tafauti na kile wanachokipata.

Maamuzi hayo ni kufuatia na matamko yaliyotolewa na Rais John Pombe Magufuli katika uzinduzi wa reli ya Standard Gauge ambapo aliwakemea vikali Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akidai kuwa taasisi hiyo inakusanya kodi kubwa ambayo hailingani na mapato wanayoyakusanya.

Ambapo katika hotuba hiyo, Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Fedha na Mipango na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha wanaondoa kero za kodi ili kutoa hamasa kwa wananchi kulipa kodi kwa manufaa ya taifa.

Video: Migos na Drake waja ‘Kizilipendwa’ kama WCB
Mwanasheria aelezea TPI ‘ilivyoiuzia’ Serikali ARV feki