Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Morogoro imekamata madumu 500 ya mafuta ya kula yakisafirishwa kwenda mikoa ya kanda ya nyanda  za juu kusini  yakitokea mkoani Tanga bila kuwa na risiti za mashine ya Kielektroniki (EFD).

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Morogoro, Maternus Shirima amesema maofisa wa mamlaka hiyo wakiwa katika operesheni ya kawaida katika maeneo mbalimbali waligundua kuwepo kwa lori lenye mafuta ambayo yaliyokuwa hayajalipiwa kodi wala kutolewa  risiti.

Amesema baada ya kukamatwa kwa lori hilo mamlaka hiyo imeanza kuchukua hatua kwa wauzaji na wanunuzi ili kuhakikisha wahusika wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria huku wakitakiwa kulipa kodi.

Amebainisha kuwa kwa sasa kumekuwa na mtindo kwa baadhi ya wanunuzi na wauzaji bidhaa kushirikishana kukwepa kulipa kodi kwa kuandikiana risiti kwa kiwango kidogo cha fedha.

Meneja huyo amesema kufanya hivyo ni sawa na kuiibia Serikali na kuikosesha mapato.

”Tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya ulipaji kodi na kudai risiti, anapotokea mtu kakiuka huwa tunachukua hatua dhidi yake kwa mujibu wa sheria yetu” amesema Shirima.

Ofisa kodi wa TRA, Peter Jacob amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanaponunua na kuuza bidhaa watoe risiti.

Amesema kwa mujibu wa sheria ya adhabu ya TRA, mtu yeyote atakayekamatwa kwa kutolipa kodi ama kutoa risiti adhabu inayomkabili ni kifungo cha miaka mitatu au kulipa faini ya Shilingi, milioni 4.5 kwa pamoja.

Serikali yabaini njia zinazotumiwa kupitisha dawa za kulevya
Dkt. Mwakyembe ayafunda mashirikisho ya Sanaa na Filamu