Mamlaka ya Mapato (TRA), imetangaza  kupiga mnada kontena 20 za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ikiwa atashindwa kuzilipia ushuru na kuzichukua ndani ya siku 30 kuanzia Jumatatu.

Kontena hizo za Makonda ambazo zimesubiri utaratibu wa kuzitoa TRA kwa zaidi ya siku 90 zinazokubalika kwa mujibu wa sheria za kodi, zimesheheni samani za ndani na ofisini.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, amesema kuwa kwa kawaida bidhaa zote zinapoagizwa na kufika bandarini zinatakiwa kuondolewa ndani ya siku 90.

Kayombo amesema inapotokea muda huo ukapita bila wahusika kuondoa mizigo yao, hujulishwa na mamlaka hiyo kwa kupewa notisi ya siku 30 ili waondoe.

Kwa mujibu wa tangazo la TRA lililotoka kwenye vyombo vya habari Jumatatu, Mamlaka hiyo imetoa notisi ya siku 30 kwa wateja nane akiwamo “Paul Makonda” ambao mizigo yao imekaa bandarini zaidi ya muda unaotakiwa.

Kayombo amesema nyaraka za bidhaa hizo ziko sawa tatizo ni muda wa kuziondoa bandarini hapo ndiyo haujafuatwa.

“Siwezi kusema kama wameshindwa kulipa kodi au la lakini hata ikitokea bidhaa ambazo zina msamaha wa kodi zimekaa zaidi ya siku zilizowekwa na wamiliki wakapewa notisi bila kutekeleza, muda wa notisi ukiisha bidhaa husika hupigwa mnada na kwenye hili hatuangalii bidhaa zimetoka wapi, ni msaada au sio msaada,” alisema Kayombo.

 

Majaliwa adai Serikali iko makini na ajira za wageni
Gianluigi Buffon atangaza kuondoka Juventus