Treni ya Kifahari ya Rovos kutoka Afrika ya Kusini imewasili jijini Dar es salaam jana ikiwa na idadi ya watalii 61 kutoka katika mataifa mbalimbali kutembelea vivutio vya kitalii nchini.

Kwa mwaka huu 2019 ni safari ya kwanza kwa treni hiyo kuleta watalii, ambapo imetumia takribani siku15, kutoka Cape town, na Watalii waliobebwa ni Waingereza, Wajerumani, Waholanzi, Wasweden, Waitaliano na watalii kutoka Afrika Kusini.

Akizungumza katika mapokezi hayo, Meneja Uhusiano wa Bodi  ya Utalii Nchini, Geofrey Tengeneza amesema ujio wa watalii hao ni fahari kubwa kwa bodi ya Utalii kwani wanatarajiwa kusambaza mema na vivutio vilivyoko Tanzania kwa wenzao.

Aidha, amesema kuwa watalii hao watagawanyika katika maeneo mbalimbali ya kitalii, ikiwemo Zanzibar, Serengeti, Ngorongoro, na sehemu nyingine zilizoko jijini Dar es salaam.

Treni ya kifahari ya Rovos imekuwa ikileta watalii nchini mara kwa mara na hupitia katika nchi za Zimbabwe, Botswana na Zambia.

Watalii hao wanatarajiwa kukaa nchini kwa siku saba wakati Treni hiyo inatarajiwa kuondoka januari 24, mwaka huu ikiwa na watalii wengine ambao walikuja mapema kwa kutumia usafiri mwingine.

Hata hivyo, takwimu kutoka sekta ya utalii nchini zinaonyesha kuwa idadi ya ujio wa watalii inaongezeka ambapo hadi kufika mwaka 2017 jumla ya watalii milioni 1.3 walifika na wengi kutoka Marekani na jumla ya dola milioni 2.2 zilipatikana na kuelekezwa katika ujenzi wa miundo mbinu ya barabara katika hifadhi za Taifa.

DC Mjema apokea jengo la Ofisi ya Walimu kutoka Serikali ya Japan
Video: Gwajima ampongeza JPM, 'Leo umekuwa Nabii'