Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewahakikishia Watanzania kuwa Mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 567.3 sawa na shilingi trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kukabiliana na athari za Uviko-19 zitasimamiwa kikamilifu ili kuleta tija iliyokusudiwa.

Akizungumza na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi Jijini Dodoma, Dkt. Nchemba amesema kuwa kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 189.1 ni mkopo nafuu usio na riba ambao umetolewa kupitia dirisha la Rapid credit Facility (RCF), na dola za Marekani milioni 378.2 ni mkopo nafuu wenye riba ndogo kupitia dirisha la Rapid Financing Instrument RFI.

Aidha fedha hizo tayari zimepokelewa nchini na zitatumika ndani ya mwaka wa fedha 2021/21 katika sekta zilizoathiriwa na UVIKO – 19 ambazo ni  afya, elimu, utalii, maji, pamoja na kusaidia kaya masikini kupitia mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

‘’Fedha hizi zitatumika katika kujenga madarasa au kujenga shule mpya ili kupunguza mlundikano wa wanafunzi darasani na kuwaepusha na maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO -19, aidha pesa hizi zitatumika katika kuongeza upatikanaji wa mitungi ya hewa ya oksijeni hasa katika hospitali zilizo pembezoni mwa mji ili kuweza kuokoa maisha ya Watanzania,” Amesema Waziri Nchemba.

Kwa upande wake Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Jamal Kassim Ali, ameishukuru Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa kuipatia Tanzania mkopo huo ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepatiwa dola milioni 100 ambazo zimeelekezwa kutumika katika sekta mtambuka zilizoathirika na UVIKO -19 hasa katika sekta ya Utalii.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bw. Jens Reinke alisema shirika hilo lipo tayari kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo nchini ili kupambana na maambukizi ya UVIKO -19 na kusaidia kukuza uchumi wa nchi.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu fedha zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ambapo shirika hilo limetoa kiasi cha sh. trilioni 1.3 ambazo zitatumika kwa Tanzania Bara na Zanzibar, jijini Dodoma.



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Jamal Kassim Ali, akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu fedha zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) ambapo shirika hilo limetoka kiasi cha sh. trilioni 1.3 ambazo zitatumika kupambana na athari za Uviko-19kwa Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi-Zanzibar, jijini Dodoma.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Jens Reinke, akieleza kwa Wanahabari kuhusu  fedha zilizotolewa na IFM kwa Tanzania ambapo alisema kuwa kiasi cha sh. trilioni 1.3 kilichotolewa na Taasisi yake kitasaidia kuimarisha uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wananchi wake..

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Septemba 16, 2021
RPC Kinondoni akana kumtesa mtuhumiwa