Aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump kupitia Chama cha Republican ameweka wazi uwezekano wa kuwania tena Urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2024 katika nchi hiyo.

Akizungumza katika mkutano wa kisiasa wa muungano wa kihafidhina (CPAC), uliofanyika mjini Orlando katika jimbo la Florida ambapo mwanachama huyo wa Republican amesema huenda akajitosa katika kinya’nganyiro cha Urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Aidha, Trump ameendelea kusisitiza madai yake kuwa alimshinda Rais wa sasa wa Marekani, Joe Biden katika uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka 2020 na kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu mkubwa licha ya kwamba hajawahi kutoa ushahidi wowote kuunga mkono madai yake.

Trump pia ametumia nafasi hiyo kukataa wito wa kuanzishwa kwa chama kipya cha kisiasa na amepuuzilia mbali ripoti za uwezekano wa kuanzishwa kwa chama cha Trump akizitaja kama habari za uwongo.

“Tukiwa pamoja katika miaka ijayo, tutaubeba na kuupeleka mbele mwenge wa uhuru wa Marekani, tutaongoza harakati za kihafidhina na chama cha Republican kurudi kwenye ushindi kamili na tumewahi kupata ushindi mkubwa, msisahau kamwe,” amesema Trump.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Machi 2, 2021
Majambazi watano wauawa, askari ajeruhiwa