Rais wa Marekani, Donald Trump ametishia kuongeza ushuru kwa bidhaa za China zenye thamani ya $200 bilioni zinazoingia nchini kwake.

Ripoti zimeeleza kuwa hatua hiyo ya Trump inaweza kuongeza uhasimu wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili zenye misuli zaidi kiuchumi duniani.

Rais Trump ameeleza kuwa China imekuwa ikinufaika zaidi kupitia biashara isiyo ya haki kati ya nchi hizo mbili, ikiingiza bidhaa zenye thamani kubwa kwa ushuru mdogo, hivyo ataongeza 10% kwenye ushuru uliopo.

Wiki iliyopita, Rais Trump alitangaza nia ya kuongeza ushuru kwa 25% kwa bidhaa za China. Lakini Beijing ilijibu mapigo kwa kutangaza kuwa endapo hilo litafanyika, na wao wataweka ushuru mkubwa kwa bidhaa 659 za Marekani zinazoingia nchini humo zenye thamani ya $50 bilioni, zinazojumuisha bidhaa za kilimo, magari na zile za baharini.

“Tamko la majibu ya china ni tishio kwa makampuni ya Marekani, wafanyakazi na wakulima ambao hawana hatia,” alisema Trump.

Trump alitoa tamko lake jana usiku akieleza kuwa amemtaka mshauri wake wa masuala ya biashara na uchumi kubainisha bidhaa za China ambazo anaweza kuziongezea ushuru zinapoingia Marekani.

“Kama China itaongeza ushuru wake tena, tutajibu kwa kuongeza ushuru kwenye bidhaa nyingine zenye thamani ya $200 bilioni. Uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na China lazima uwe na usawa zaidi,” alisema Trump.

Habari kubwa katika magazeti ya leo Juni 19, 2018
JPM amteua Jaji Lubuva