Rais wa Marekani, Donald Trump ameiwekea kiunzi kingine Serikali ya Zimbabwe baada ya kupitisha sheria inayoweka masharti ili nchi hiyo iweze kuondolewa vikwazo vya kiuchumi.

Sheria hiyo iliyosainiwa na Trump inaweka sharti kuwa Jeshi la Zimbabwe lazima liheshimu haki za binadamu na uhuru wa kila mtu na pia kutojihusisha na masuala ya kisiasa.

Kadhalika, sheria hiyo iliyosainiwa Ijumaa iliyopita inaeleza kuwa ili Zimbabwe iondolewe vikwazo, uchaguzi wa Julai 30 ni lazima ukubalike kwa wazi kuwa ulikuwa ni uchaguzi huru na haki.

Ingawa Rais Emmerson Mnangagwa amekaririwa akieleza kuwa Zimbabwe iko wazi kwa ajili ya biashara na nchi nyingine, sheria hiyo itakuwa kisiki kingine dhidi ya ndoto yake ambacho hanabudi kukivuka.

Wakati hayo yakiendelea, chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe cha Movement for Democratic Change (MDC) kimefungua kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu.

MDC wanaamini kuwa mgombea wao Nelson Chamisa alishinda na hawayatambui matokeo ya Tume ya Uchaguzi yaliyompa Mnangagwa  wa Zanu-PF ushindi wa 50.8%.

Watu 6 wameripotiwa kuuawa wakati jeshi la nchi hiyo lilipoingia barabarani kuwazuia wafuasi wa chama cha upinzani kuandamana kupinga matokeo.

LIVE: Katibu Mkuu CCM azungumza na vyombo vya habari, Mbunge mwingine upinzani ajiuzulu
Mfanyakazi aiba ndege Bombardier Q400, aiangusha

Comments

comments