Wabunge wa Chama Cha Democratic wameendelea kumkalia kooni Rais wa Marekani, Donald Trump ikiwa ni saa chache baada ya kuwekwa wazi kwa ripoti kuhusu sakata la tuhuma za Urusi kuingilia uchaguzi wa nchi hiyo mwaka 2016.

Democratic inamtaka Robert Mueller ambaye aliiandaa ripoti hiyo kufika mbele ya bunge kwa ajili ya kutolea ufafanuzi mambo kadhaa yaliyoibuliwa kwenye ripoti yake.

Ripoti hiyo ambayo iliachiwa Alhamisi wiki hii, imeeleza kuwa hakukuwa na ushahidi wa wazi kuwa Trump na timu yake walishirikiana ki-jinai kwenye uchaguzi huo uliompa ushindi.

Timu ya wanasheria wa Trump wameielezea ripoti hiyo kama ushindi mkubwa dhidi ya sakata ambalo limekuwa gumzo duniani kote.

Hata hivyo, Katika Ripoti hiyo, imeelezwa kuwa kuna wakati Rais Trump alitaka kumfukuza kazi Mueller wakati akiendelea na uchuguzi wake, hali iliyotafsiriwa na baadhi ya watu kuwa alitka kuingilia uchunguzi huo.

Ripoti hiyo yenye kurasa 448 ni matokeo ya kazi iliyofanywa na Mueller na timu yake kwa miezi 22. Mueller aliteuliwa kufanya kazi ya kuchunguza sakata la Urusi kuingilia uchaguzi wa mwaka 2016 pamoja na kufahamu kama nchi hiyo ilishirikiana na timu ya Trump wakati wa kampeni.

Ingawa chama hicho kimeendelea kumuandama Trump hata baada ya ripoti hiyo, hali halisi inaonesha kuwa Rais huyo anaendelea na mbio za uongozi akiwaachia wapinzani wake vumbi tu.

Lissu akunja mamilioni ya posho, mishahara ya miezi mitatu
Serikali ya Mali yajiuzulu, umma waikataa