Rais wa Marekani, Donald Trump amepokelewa na maandamano ya mamia ya watu wanaomuunga mkono na wasiomuunga mkono alipotembelea maeneo ya Dayton, Ohio na El Paso, Texas leo ikiwa ni siku nne baada ya mashambulizi yaliyofanywa kwa nyakati tofauti na vijana wadogo waliojihami kwa bunduki na kuua jumla ya watu 31.

Trump na mke wake Melania wametembelea hospitali moja ya Dayton, Ohio ambapo watu 9 waliuawa na kijana mmoja aliyejihami kwa bunduki ya kivita. Walitumia muda mrefu kuzungumza na wahudumu wa hospitali pamoja na wahanga wa tukio hilo, kwa mujibu wa CNN.

Kwa mujibu wa polisi, mshambuliaji wa Dayton anadaiwa kuwa alivaa vazi la kuficha sura (mask), nguo maalum ya kuzuia risasi kupenya (bullet proof), na alitumia bunduki ya kivita. Aliwaua watu 9 papo hapo akiwemo dada yake na kuwajeruhi vibaya watu 16. Polisi wanaeleza kuwa walifanikiwa kumuua ndani ya sekunde 30 tangu alipoanza kufyatua risasi.

Lakini pia, kijana mwingine, Patrick Crusius mwenye umri wa miaka 21 aliua watu 22 na kujeruhi wengine 24 katika eneo la El Paso, Texas baada ya kufyatua risasi kadhaa kwa kutumia bunduki aina ya AK. Tukio hilo lilihusishwa na ubaguzi wa rangi baada ya polisi kueleza kuwa saa chache kabla ya kutekeleza shambulizi hilo, Patrick aliandika kwenye mtandao wa kijamii ujumbe wa kibaguzi akieleza kupinga kile alichokiita uvamizi wa wahamiaji katika jimbo la Texas.

Kwa mujibu wa shirika la habari la DW, mamia ya watu waliandamana barabarani kupinga ziara hiyo ya Trump ambaye baadhi yao wanamtuhumu kwa kutoa kauli zinazohusishwa na ubaguzi wa rangi.

Waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yaliyomtaka Rais huyo kukishinikiza Chama kinachotetea umiliki wa bunduki Marekani (NRA) kusitisha uuzaji wa silaha hizo.

Siku nne zilizopita, mtu mmoja aliyejihami alifyatua risasi na kuwaua watu wanne katika eneo hilo, katika tukio ambalo linadaiwa kuchochewa na sababu za kiubaguzi wa rangi.

 

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 9, 2019
Uongozi wa 2Baba wazungumzia afya yake, kukimbizwa hospitalini