Rais wa Marekani, Donald Trump amepinga kauli ya mshauri wake mkuu wa masuala ya ulinzi, John Bolton aliyedai kuwa mfumo wa kuondoa silaha za kinyuklia nchini Korea Kaskazini utafanana na uliotumika Libya.

Tump amesisitiza kuwa makubaliano kati ya Marekani na Korea Kaskazini yanayotarajiwa kuanza katika mkutano kati ya viongozi wa nchi hizo mbili, uliopangwa kufanyika Juni 12 mwaka huu hayana mlengo wowote wa mfanano na aliyoyasema Bolton.

“Mfumo uliotumika Libya sio mfumo ambao tunaulenga tunapofikiria suala la Korea Kaskazini,” alisema Trump.

Rais Trump alifafanua kuwa anachofikiria ni kuhakikisha Korea Kaskazini inafuata mfumo wa Korea Kusini katika kuleta maendeleo baada ya kuondolewa vikwazo. Aliwasifu watu wa Korea Kaskazini kuwa ni watu wazuri na wachapakazi, hivyo anaamini baada ya makubaliano hayo yatakayoondoa vikwazo pia nchi hiyo itakuwa tajiri zaidi.

Korea Kaskazini ilitishia kuachana na mpango wa kiongozi wake, Kim Jong-un kufanya mazungumzo na rais Trump nchini Singapore baada ya kukasirishwa na kauli za Bolton pamoja na mazoezi ya pamoja kati ya Marekani na Korea Kusini ambayo waliyataja kuwa ni mazoezi ya kujiandaa kufanya uvamizi.

Mwaka 2003, Libya chini ya uongozi wa Muammar Gaddafi ilitangaza kuachana na mpango wake wa kutengeneza silaha za maangamizi za kinyuklia, hatua iliyoishtua dunia. Uamuzi huo ulisababisha kuondolewa vikwazo pamoja na kurejeshwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati yake na Marekani pamoja na washirika wake.

Hata hivyo, mwaka 2011, Libya ilivamiwa na waasi walioungwa mkono na Marekani chini ya mwamvuli wa NATO na mwisho wakamuua Gaddafi.

Historia hiyo imemshtua Kim Jong-un ambaye alitangaza kuteketeza vinu na eneo la majaribio la silaha za maangamizi za kinyuklia za nchi hiyo.

Hata hivyo, kuna mkanganyiko wa matakwa ya Marekani na inachofanya Korea Kaskazini, ambayo imesema kuwa katika makubaliano yake na Korea Kusini, walikubaliana kuharibu na kuachana na mpango wa silaha za nyuklia katika eneo lote la Rasi ya Korea, kwa pande mbili.

 

Ben Pol aweka wazi atakavyofunga ndoa ‘kimaajabu’
Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Mei 18, 2018