Rais wa Marekani, Donald Trump amemjibu rapa Jay Z kwa kile alichokisema kwenye mahojiano na CNN kuhusu matamshi ya kibaguzi yanayodaiwa kutolewa na kiongozi huyo.

Akizungumza katika mahojiano maalum kwenye kipindi cha The Van Jones Show wiki hii, rapa huyo nguli ambaye jina lake halisi ni Shawn Carter alikosoa vikali matamshi yanayodaiwa kuwa ya Trump akiizita nchi za afrika kuwa ni nchi chafu (nchi za shimo la choo).

“Ndiyo, inaumiza sana na inatuangusha. Kila mtu alisikia hasira. Baada ya hasira inaumiza kweli kama mtu anawadharau watu wote,” alisema na kuongeza kuwa ingawa amekanusha matamshi hayo, hivyo ndivyo watu humzungumzia.

Rapa huyo alienda mbali akimkosoa Trump kwa vitendo vya kibaguzi na kumuita kuwa ni mdudu aliyeshindikana kwa dawa (superbug).

Alipinga kauli kuwa Marekani sasa imeongeza idadi ya ajira hasa kwa nchi za Afrika kama inavyodaiwa na Serikali ya Trump.

Leo, Trump ametumia mtandao wa Twitter kama ilivyo kawaida yake na kumjibu Jay-Z akimtaja jina, akisisitiza kuwa tangu aingie madarakani idadi ya Wamarekani Weusi wasio na ajira imeshuka.

“Mtu mmoja amtaarifu Jay –Z tafadhali kwamba kwa sababu ya sera zangu, idadi ya watu weusi wasio na ajira wameripotiwa kuwa katika KIWANGO CHA CHINI KUWAHI KUTOKEA,” inasomeka tweet ya Trump.

Gambo atumbua wawili Arusha
Wastara awajibu waliomuita tapeli