Rais wa Marekani, Donald Trump amemtumia ujumbe wa heri na wa mualiko, Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un akimtaka wakutane kwenye mpaka wa nchi za Korea ambapo anaenda kukutana na Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in.

Trump ametumia mtandao wa Twitter kufikisha ujumbe wake kwa Kim Jong Un, akieleza kuwa angependa kumshika mkono na kumsalimia ‘hello’.

Rais huyo wa Marekani amepanga kuitembelea Korea Kusini baada ya kushiriki mkutano wa G20 nchini Japan, ambapo alifanya mazungumzo na Rais wa Urusi, Vladimir Putin na Rais wa China, Xi Jinping.

“Baada ya kufanya mikutano muhimu sana, ikiwa ni pamoja na Rais Xi wa China, nitakuwa naondoka Japan kwenda Korea Kusini na Rais Moon. Nikiwa kule, kama Mwenyekiti Kim [Jong-Un] anaona hii, ningependa kukutana naye kwenye mpaka ili nimsalimie na  kumshika mkono ‘Hello’,” ameandika Trump.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya Reuters, Korea Kaskazini imeelezea ujumbe wa Trump kama ‘pendekezo zuri sana’.

Kufuatia mkutano wa G20 (mataifa 20 yenye nguvu), Trump atafanya mazungumzo na Rais wa Korea Kusini katika eneo la Seoul ikiwa ni pamoja na kuhusu mpango wa Korea Kaskazini kuachana na utengenezaji wa silaha za nyuklia.

Trump na Kim wameshakutana mara mbili, na mkutano wa pili uliofanyika Februari nchini Vietnam ulivunjika baada ya kutokubaliana katika hatua za awali.

LIVE DODOMA: Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Taifa ya TAKWIMU
Video: Naibu Meya Ilala na wananchi wapeana ya papo kwa papo