Rais wa Marekani, Donald Trump amevipongeza vikosi vya Marekani na washirika wake Uingereza na Ufaransa kwa jinsi vilivyotekeleza mashambulizi ya kuiadhibu Syria yaliyodumu kwa takribani saa 12.

Kwa mujibu wa ripoti, vikosi vya majeshi hayo vilirusha makombora mazito 100 kwenye maeneo ambayo wanadai ndiko kuna silaha za kemikali.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Trump ambaye awali aliwashukuru Uingereza na Ufaransa kwa kushiriki katika mpango huo, amesema mashambulizi hayo yametekelezwa na kukamilika kwa ukamilifu stahiki.

Hata hivyo, Rais wa Urusi, Vladimir Putin ambaye vikosi vyake viko nchini Syria vikiisaidia Serikali ya nchi hiyo kupambana na waasi pamoja na magaidi, ametoa onyo kali dhidi ya mashambulizi hayo ya Marekani na washirika wake.

Rais Putin amesema kuwa analaani vikali mashambulizi hayo na anaonya kuwa nchi yake itajibu mapigo kijeshi endapo mtumishi yoyote wa Urusi aliyeko nchini Syria atapata madhara yanayotokana na mashambulizi ya nchi hizo za Magharibi.

Haya ni mashambulizi makubwa zaidi kuwahi kufanywa na Marekani dhidi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad tangu kuzuka kwa vita nchini humo, miaka saba iliyopita.

Assad amesema kuwa mashambulizi hayo yanazidi  kuwaimarisha wananchi na serikali yake katika kuhakikisha inaendelea kupambana na ugaidi wa aina yoyote katika eneo lolote nchini humo.

Marekani na washirika wake wanaishutumu Syria kwa kutumia silaha za kemikali katika eneo la Douma hali iliyosababisha vifo na madhara makubwa ya kiafya kwa wananchi.

Kikwete ampa neno Alikiba kuhusu ndoa yake
Wananchi Makowo wajenga kituo cha afya

Comments

comments