Rais mteule wa Marekani, Donald Trump jana alitoa kauli zilizowaacha wengi mdomo wazi, muda mfupi baada ya kuteta kwa dakika 90 na Rais wa Marekani, Barack Obama ndani ya Ikulu ya nchi hiyo.

Wakizungumza kwa ufupi mbele ya waandishi wa habari ndani ya ‘White House’ kuhusu mazungumzo yao, Trump mbaye katika kampeni zake alionekana kumshambulia Obama akitilia mashaka uraia wa Rais huyo pamoja na kukosoa vikali uongozi wake, alionekana kubadili upepo.

Trump aliwaambia waandishi wa habari kuwa Rais Obama ni ‘mtu mwema sana’ na kwamba wamezungumza mambo mengi muhimu yatakayosaidia kuendeleza ‘kazi nzuri’ aliyokwisha ifanya pamoja na kumuomba ushauri.

“Rais [Obama], ni heshima kubwa kuwa na wewe na ninatarajia kuwa nawe tena mara nyingi zaidi… ikiwa ni pamoja na kukuomba ushauri,” alisema Trump na kuongeza kuwa katika mazungumzo yao wamezungumzia mambo mazuri sana.

Kauli hizo za Trump zilizua mjadala, wengi wakianza kuhisi huenda akabadili msimamo wake kwa mambo mengi aliyowahi kuyazungumza yenye utata wakati wa kampeni zake.

Rais Obama alimhakikishia ushirikiano ili kufanikisha na kumueleza kuwa endapo atafanikiwa yeye ina maana Marekani imefanikiwa.

“Tumezungumza mengi kuhusu sera za ndani na sera za kimataifa pamoja na kuiweka pamoja Marekani,” alisema Obama.

Obama pia alisema kuwa Trump amemhakikishia kuwa ataitumia timu [ya Obama] katika mambo mengi kupata uzoefu kwa ajili ya mafanikio ya taifa hilo kubwa duniani.

Obama anatarajiwa kumkabidhi rasmi Trump kijiti cha Urais, Januari 20 mwakani.

Stefano Pioli Kumsajili Matteo Darmian
Tanzia: Mbunge Hafidh Ali wa Jimbo la Dimani afariki dunia