Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema kikosi chao kipo tayari kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans utakaopigwa Jumamosi (Desemba 11) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

‘Try Again’ ametoa kauli hiyo akiwa mjini Lusaka, Zambia ambako kikosi cha Simba SC jana Jumapili (Desemba 05) kilikabiliwa na mchezo wa Mkondo wa Pili wa Kombe la Shiriksiho Afrika dhidi ya Red Arrows.

Kiongozi huyo amesema kikosi chao msimu huu kipo tayari kwa mchezo wowote, huku akiwatoa hofu Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kuelekea Jumamosi (Desemba 11).

“Niwatoe wasiwasi Mashabiki na Wanachama wa Simba SC, timu yao ni nzuri, inaweza kukabiliana na yoyote msimu huu, tunakwenda kucheza na timu ya kawaida ambayo ipo kwenye Ligi kama ilivyo kwa timu nyingine,”
“Sioni shaka, Sioni wasiwasi kwa nini tunazungumzia mchezo unaofuata, huo ni mchezo kama mchezo mwingine wowote wa Ligi tuliowahi kucheza ama tutakaocheza msimu huu.”

Hakuna sababu ya kuhofia, sisi Simba SC sio watu wa tambo wala Sio watu wa kujivuna, lakini tunachosema ni kwamba tunakwenda kushinda mchezo huo. Sisi kila mchezo ambao tunakutana na mpinzani yoyote tunahakikisha kwamba tunashinda.” amesema Try Again

Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 17, ikitanguliwa na Young Africans yenye alama 19, huku kila timu ikicheza michezo saba hadi sasa.

Idriss Mbombo aitahadharisha Kagera Sugar
Mwakalebela aichimba MKWARA Simba SC