Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema wanasubiri ripoti ya Kocha Mkuu Pablo Franco Martin, ili kufahamu kama anahitaji kufanya usajili wakati wa Dirisha Dogo.

Msimu wa usajili wa Dirisha Dogo unatarajiwa kuanza rasmi Desemba 15 na kufikia tamati Januari 15-2022.

‘Try Again’ amesema usajili wa wachezaji kupitia Dirisha Dogo ndani ya klabu ya Simba utategemea na ripoti ya Kocha huyo kutoka nchini Hispania, ambaye amechukua nafasi ya Kocha Didier Gomes aliyeondoka mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Amesema wao kama viongozi hawana mamlaka yoyote ya kufanya usajili bila kupata ripoti ya Benchi la Ufundi, hivyo amewahimiza Mashabiki na Wanachama kuendelea kuwa watulivu.

“Tunasubiri Ripoti ya Kocha wetu, kama atahitaji kufanya usajili tutamtimizia hitaji hilo, tunaamini katika taaluma yake ambayo itamuonyesha wapi pamepungua ili kuongeza makali ya kufikia lengo tuliojiwekea msimu huu.” amesema Tyr Again

Kuhusu fedha za usajili kiongozi huyo amesema, klabu ya Simba ina fedha za kutosha kufanya usajili wa mchezaji yoyote atakaependekezwa na Kocha Mkuu, hivyo wamejipanga kwa kila kitu.

“Fedha ya usajili ipo, tuna uwezo wa kumsajili mchezaji yoyote kwa sasa, iwe hapa Tanzania ama nje ya Tanzania, tunachosubiri kwa sasa ni Ripoti ya Kocha kama itaturuhusu kufanya hivyo mtaona nguvu ya fedha iliopo Simba SC.”

Mbali na kutoa uhakika huo, kiongozi huyo jana Jumapili (Novemba 22), alihutubia kwenye Mkutano Mkuu wa Wanachama na kugusia suala la Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Zambia na klabu ya RS Berkane ya Morocco Clatous Chotta Chama ambaye anahusishwa kurudia Tanzania.

Try Again alisema: “Mimi siwezi kumsemea Chama ni mchezaji bado ana mkataba na Berkane, sisi tumemuuza kwenda klabu ile, lakini moja ya masharti ya mkataba ule ni kwamba atakaposhindwa kule basi atarudi kwenye Klabu yetu ya Simba. Kwa hiyo kama yeye Chama anaona hana furaha mimi sina taarifa hizo, kama yuko tayari basi anakaribishwa Simba. Simba ni nyumbani kwake, wakati wowote atakuja kucheza mpira kwenye klabu hii.”

Rais Samia mgeni rasmi siku ya ukimwi duniani
Kaze awashtua wachezaji Young Africans