Kiungo mkabaji wa AS Vita Club Papy Kabamba Tshishimbi  ameichimba mkwara Simba SC kuelekea mchezo wa mzunguuko watano wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Makundi utakaochezwa April 03, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Tshishimbi ambaye alijiunga na AS Vita Club mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuachana na Young Africans, amesema watakuja Tanzania kupambana na wanaamini hakuna kitakachowasimamisha kufikia lengo la ushindi kwenye mchezo huo.

Amesema wanafahamu Simba SC watahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kujihakiishai nafasi ya kutinga hatua ya Robo Fainali, lakini  AS Vita Club ina malengo zaidi ya hayo kwenye uwanja wa ugenini.

“Tuna michezo miwili imebaki kukamilisha ratiba ya hatua hii ya makundi, na ili kufuzu robo fainali ni lazima tushinde michezo hiyo dhidi ya Simba na Al Merrikh, hivyo tutajitahidi kufanya hivyo Yaani kiufupi Afe kipa Afe beki lazima wafe pale pale kwenye uwanja wao wa nyumbani, kwanza tuna hasira nao sana walitudhalilisha kwenye uwanja wetu” amesema Papy Tshishimbi.

Kwa upande wa AS Vita watahitaji kuutumia mchezo huo kama sehemu ya kulipa kisasi cha kufungwa nyumbani kwenye mchezo wa mzunguuko wa kwanza, ambapo Simba waliibuka na ushindi wa 1-0, mjini Kinshasa, DR Congo.

Hata hivyo hii haitokua mara ya kwanza kwa AS Vita kucheza Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam, kwani kamaitakumbukwa vyema timu hiyo inayonolewa na Florent Ibenge ilipoteza mbele ya Simba SC msimu wa 2018/19 kwa kufungwa 2-1, na kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Makundi.

Mpaka sasa Simba SC inaongoza msimamo wa ‘Kundi A’ la michuano hiyo wakiwa wamejikusanyia alama 10, wakifuatiwa na mabingwa watetezi wa michuano hiyo Al Ahly wenye alama 7, AS Vita wao wako kwenye nafasi ya tatu na alama 4, huku Al Merrikh ya Sudani wao wakiburuza mkia na alama 1.

Namungo FC yaiwekea mikakati Nkana FC
Dkt. Abbas: Ndoto za Magufuli zitatekelezwa